Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amewashauri watanzania kuenzi,kutunza na kuendeleza urithi wa utamaduni wa asili kwa ajili ya manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Kanali Thomas ametoa ushauri huo wakati anafungua Tamasha la miaka 119 ya kumbukizi ya mashujaa wa vita ya Majimaji na utalii wa utamaduni kwenye viwanja ya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji mjini Songea.
Ameutaja urithi wa utamaduni kuwa ni tunu na kioo cha Taifa la Tanzania na kwamba unaleta umoja,amani na mshikamano wa kitaifa ikiwa ni Pamoja na kulitambulisha Taifa la Tanzania Duniani.
“Natoa rai kuendelea kuibua na kuendeleza fursa za utalii wa utamaduni zinazopatikana katika Mkoa wa Ruvuma na Ukanda wa Kusini kwa ujumla ili kuinua Uchumi na kuboresha hali ya Maisha ya wananchi wa eneo hili’’,alisisitiza RC Thomas.
RC Thomas ameutaja Mkoa wa Ruvuma kuwa ni miongoni mwa mikoa michache nchini ambao umejaliwa kuwa na ardhi yenye rutuba,madini,mito hifadhi za wanayamapori na vivutio vingine vinavyoweza kuchochea maendeleo ili kuuvusha Mkoa kutoka sehemu moja na Kwenda sehemu nyingine.
Akizungumzia tamasha hilo,Mkuu wa Mkoa amesema kila mwaka kuanzia Februari 23 hadi 27 linafanyika tamasha la kumbukizi ya mashujaa wa vita ya Majimaji wakikumbukwa mashujaa 67 walionyongwa mjini Songea na wajerumani Februari 27,1906 ,wakitetea maslahi ya nchi ya Tanganyika.
Kwa upande wake Kaimu Mhifadhi wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Rozi Kangu akitoa taarifa ya makumbusho ya kumbukumbu ya vita ya Majimaji,amesema historia hiyo inaanzia mwaka 1905 hadi 1907 baada ya mashujaa 67 kukamatwa na kunyongwa kikatili na wajerumani kisha kuzikwa kwenye makaburi mawili yaliyopo ndani ya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji.
Amesema makumbusho ya Majimaji yalianzishwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Hayati Dkt.Lawrence Gama mwaka 1980 na mwaka 2009 makumbusho hayo yalikabidhiwa kwa Shirika la Makumbusho ya Taifa kwa mujibu wa sheria ya makumbusho ya Taifa namba 7 ya mwaka 1980.
Amesema kilele cha maadhimisho hayo ni Februari 27,2024 ambapo Februari 24,2024 yatafanyika mashindano ya ngoma za asili kutoka Halmashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma na Februari 25,2024 litafanyika kongamano la kurithisha urithi wa utamaduni mjini Mbambabay wilayani Nyasa.
Naye Chifu wa Tano wa Kabila la Wangoni Nduna Emanuel Zulu Gama amesema katika maadhimisho ya mwaka huu amewaalika machifu kutoka nchini Malawi na mikoa mingine ambayo ni Njombe,Iringa,Tabora,Mwanza,Lindi na Mtwara.
Kaulimbinu ya kumbukizi ya mashujaa wa vita ya Majimaji mwaka huu ni Majimaji ni ukombozi wa Bara la Afrika na matumizi ya rasilimali zake ni urithi wetu kwa maendeleo ya utalii na Uchumi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.