Shirika lisilokuwa la kiserikali la kuhudumia watu wasiojiweza na wenye Ulemavu (PADI) linatarajia kuanza kutoa mafunzo ya kupinga ukatili wa kijinsia kwa watoto wa kiume wenye umri wa miaka tisa hadi 14 katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.
Meneja Mradi wa PADI Gifti Kilasi amesema kupitia mradi wa USAID KIZAZI KIPYA unnaoratibiwa na PADI,utaanza kutoa mafunzo kwa watoto hao ili waweze kufahamu madhara ya ukatili wa kijinsia na waanze kupinga ukatili huo katika jamii.
Kwa mujibu wa Meneja huyo, Mradi huo umeanza kutekelezwa mwaka 2017 na unatarajia kukamilika mwaka 2021 na kwamba hadi sasa wamesajili watoto 900 wa shule za Msingi na lengo ni kuwafikia watoto 8000 katika Mkoa wa Ruvuma hadi kufikia Septemba 2021.
Ameongeza kuwa wamegeukia kundi hilo kwa sababu ni wahanga wa ukatili wa kijinsi,na kwamba kundi hilo lilisahaulika katika kuwapa elimu ya kupambana na ukatili wa kijinsia ukilinganisha na watoto wa kike.
Afisa Ustawi wa Halmashauri ya Wilaya ya songea Suzana Mkondya amewaasa wazazi na walezi kutoa taarifa pale watoto wa kiume wanapofanyiwa vitendo vya ukatili katika jamii.
Amesema baada ya mafunzo hayo wanatarajia matendo vitendo vya ukatili vitapungua kwa kiasi kikubwa na watoto wataelimika na kuanza kutoa elimu kwa vijana wengine.
Hata hivyo amesema mafunzo hayo yatatolewa kwa nadharia na vitendo kupitia michezo na kwamba yatafundishwa na walimu wa shule za msingi katika maeneo husika na watoto watapata fursa ya kupima afya zao bure.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Zena Ibrahimu ametoa wito kwa wadau wa mradi huo kusimamia vizuri na kutoa ushirikiano wa dhati katika utekelezaji wa mradi huo ili uweze kutoa matokeo chanya ya kujenga na kulinda maadili mema ya kitanzania.
Ibrahimu amewataja Watoto watakaofaidika na mafunzo hayo wanatoka katika Kata za Parangu, Maposeni, Kilagano, Litapwasi, Mpitimbi, Kizuka,Litisha,Magagula,Peramiho na Mbinga mhalule na kwamba kila kata zimechaguliwa shule tatu na kila shule wamechaguliwa wanafunzi 30.
Imeandikwa na Jakline Clavery
Afisa Habari Halmashauri ya Wilaya ya Songea
Septemba 15,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.