Watoto wawili waliotoroshwa kutoka kijiji cha Mkowela, wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma na kupelekwa nchini Msumbiji kwa ajili ya kufanyishwa kazi, wamefanikiwa kurejeshwa nyumbani salama baada ya juhudi za serikali kushirikiana na wazazi wao.
Afisa Mtendaji wa kijiji cha Mkowela, Bi. Regina Duwe alisema watoto hao walichukuliwa kimya kimya tarehe 10 Februari na kupelekwa nchini Msumbiji.
Hata hivyo, juhudi za uongozi wa mkoa wa Ruvuma, ziliwezesha kurejeshwa kwao salama.
Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Afisa Malalamiko wa Mkoa, Bi. Amina Tindwa, alifika eneo la tukio ili kuhakikisha watoto hao wanarejea salama na kushuhudia hatua zinazochukuliwa kuhakikisha wanalindwa.
“Hawa ni watoto wadogo ambao wanapaswa kupata haki yao ya msingi, ikiwemo elimu, badala ya kufanyishwa kazi,” alisema Bi. Tindwa.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkowela, Bw. Saidi Ashimu Mauridi, amepongeza juhudi za uongozi wa mkoa na serikali kwa kuhakikisha watoto hao wanapatikana.
“Ni tukio baya kwa watoto wadogo kama Devotha na Novisiana kutoroshwa na kufanyishwa kazi zisizofaa “,alisema.
Kwa upande wao, wazazi wa watoto hao, akiwemo Bw. Adam Kasomwa, wameishukuru serikali kwa jitihada zake na kuhakikisha watoto wao wanarejea nyumbani wakiwa salama.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.