WAZAZI wametahadharishwa kuzingatia usalama wa mtoto katika ulimwengu wa kidijitali kutokana na takwimu hapa nchini kuonesha kuwa asilimia 67 ya Watoto wenye umri kuanzia miaka 12 hadi 17 wanatumia mitandao bila usimamizi.
Tahadhari hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mheshimiwa Kapenjama Ndile katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika,kimkoa yamefanyika katika uwanja wa Rwinga mjini Namtumbo.
Kanali Thomas amesema takwimu zinaonesha kuwa katika kila nchi duniani,Watoto ndiyo kundi linaloongoza kwa utumiaji wa bidhaa za mawasiliano bila kuzingatia matumizi sahihi.
Amebainisha zaidi kuwa Watoto wengi wanatumia mitandao mbalimbali ikiwemo simu za ndugu zao,walezi,wazazi na marafiki hivyo ametoa rai kwa jamii kuhakikisha Watoto wanaelekezwa kuzingatia matumizi sahihi na salama dhidi ya vifaa vya kieletroniki kutokana na kasi ya uwepo wa vitendo vya ukatili vinavyofanyika mtandaoni.
Ametoa rai kwa kila mzazi na mlezi kuhakikisha mtoto hatumii vifaa vya kieletroniki kama simu,intaneti na luninga bila uangalizi wa karibu ili kumepusha kujiingiza kwenye maeneo hatarishi ya kufanyiwa ukatili wa mtandaoni.
“Mkoa wa Ruvuma na mikoa mingine nchini,bado tunakabiliwa na vitendo vya ukatili wa aina mbalimbali ikiwemo ubakaji,ulawiti,utumikishaji katika ajira hatarishi,ndoa na mimba za utotoni’’,alisisitiza.
Hata hivyo Kanali Thomas,amekemea tabia ya baadhi ya wanaume kurithi wajane na kutelekeza Watoto kwa kuwaacha wanaangaika bila huduma za msingi ambapo amesema vitendo hivyo vimekithiri na kuendelea kuripotiwa katika vituo vya polisi,ustawi wa jamii na katika ngazi zote za kaya,Kijiji,kata,wilaya hadi mkoa.
Ametoa rai kwa viongozi wote wa serikali na madhehebu ya dini kuwajibika kwa kuwalinda Watoto na kuwapeleka shule,kuwalea na kuwapa haki zao za msingi kama chakula,matibabu.malezi bora na kuwalinda dhidi ya unyanyasaji.
Amesema Mkoa wa Ruvuma unaendelea kutoa huduma mbalimbali kwa watoto ikiwemo elimu kwa Watoto kuanzia shule za awali,msingi,sekondari hadi vyuo vikuu na kutoa huduma ya afya zikiwemo chanjo kwa Watoto ili kuepuka maradhi na kuwa na afya bora.
Awali akisoma risala ya maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika,mwanafunzi wa shule ya msingi Namtumbo Amina Said alisema maadhimisho hayo yanafanyika kila mwaka Juni 16,kuendeleza kumbukumbu ya mauaji ya Watoto zaidi ya 600 yaliyofanywa na makaburu katika kitongoji cha Soweto nchini Afrika ya kusini Juni 16,1976.
Watoto hao wa kiafrika waliuawa baada ya kuandamana ili kudai haki zao za msingi kama vile kutobaguliwa katika mfumo wa kupata elimu,afya na kunyanyaswa na makaburu.
Hata hivyo katika risala hiyo Watoto hao wameishukuru serikali ya Awamu ya Sita kwa kiwango kikubwa kuwapatia Watoto wa Tanzania fursa sawa katika masuala mbalimbali yakiwemo elimu,afya na ulinzi kuanzia ngazi ya familia,wilaya hadi mkoa
Kauli mbiu ya maadhimisho ya maadhimisho ya siku yam toto wa Afrika 2023 ni zingatia usalama wa mtoto katika ulimwengu wa kidijitali.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.