WAZIRI wa nchi ofisi ya Rais menejimenti ya utumishi wa umma na utawala Bora Jenista Mhagama,amezindua rasmi Hoteli ya kisasa ya CANOPIES iliyopo mtaa wa Making’inda Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo Waziri Mhagama,amewaomba wafanyabiashara wa ndani na nje kuja kuwekeza zaidi mkoani Ruvuma kwenye sekta ya utalii na Hoteli kwani mkoa huo ni eneo bora na salama kwa ajili ya kuwekeza kutokana na kuwa na vivutio vingi vya utalii ikilinganisha na maeneo mengine hapa nchini.
Alisema,serikali ya awamu ya sita itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji huku akiwataka wakazi wa mkoa wa Ruvuma hususani vijana kujifunza kwa vijana kutoka mikoa mingine walioamua kuwekeza miradi ya maendeleo mkoani Ruvuma badala ya kukimbilia kwenda maeneo mengine.
Alisema,mkoa wa Ruvuma bado kuna fursa kubwa ambayo zinahitaji kuwekezwa hasa kwenye miradi mbalimbali itakawezesha kubadilisha taswira ya mkoa huo unaotajwa kuwa na vivutio mbalimbali vya utalii ikiwamo ziwa nyasa,hifadhi ya Taifa ya Nyerere na meoneo mengine yanye utajiri ambayo bado hajafanyiwa kazi.
“kuna tatizo kubwa la ajira katika mkoa huo wetu,kwa hiyo tukifungua miradi kama hii itawezesha kusaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana wetu wa mkoa wa Ruvuma na kupanua wigo wa ulipaji kodi kwa serikali”alisema Mhagama.
Alisema,uwekezaji huu wa Hoteli ya Canopies unakwenda kufungua shughuli za kiuchumi katika manispaa ya Songea na mkoa wa Ruvuma na kuwataka viongozi wa mkoa wa Ruvuma kuwatambua,kuwasaidia na kuwaunganisha vijana wa mkoa huo na taasisi za fedha zinazoweza kutoa mikopo rahisi na yenye riba nafuu.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa huo Kanali Laban Thomas alisema,ufunguzi wa Hoteli ya Canopies ni mafanikio ya mwaka mmoja wa uongozi wa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Suluhu Hassan.
Amempongeza Mkurugenzi wa Hoteli hiyo Desdery Rutta, kwa uthubutu wake wa kujenga Hoteli ya kisasa ambayo inakwenda kuongeza idadi ya nyumba za kulala wageni katika mkoa wa Ruvuma na kutoa wito kwa vijana wengine kuiga mfano huo.
Alisema,ujenzi wa Hoteli hiyo mbali na kutoa ajira kwa vijana wa mkoa wa Ruvuma pia itaongeza wigo wa usimamizi wa mapato na ukusanyaji wa kodi za serikali ili kwenda sambamba na malengo ya serikali yetu.
Akizungumzia juu ya ujenzi wa barabara ya lami kutoka eneo la Ottawa hadi Hotelini hapo Mkuu wa mkoa alisema, tayari serikali iko katika hatua ya mwisho ya kujenga barabara ya lami kutoka Seed farm hadi uwanja wa ndege km 26 ambayo itapita kando kando ya Hoteli hiyo.
Awali Mwakilishi wa Hoteli hiyo Veronica Gondwe alisema, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa sekta ya utalii jambo ambalo limekuja wakati muafaka kwao.
Alisema,ujenzi wa Hoteli ya Canopies ulianza rasmi mwaka 2014 ikiwa ni katika juhudi za uwekezaji wa ndani na nje kwa kuzingatia kuwa imejengwa karibu na mlima Chandamali ambao una vivutio vya aina yake kama vile pango la kale,miti ya asili na nyuki wapole wasiouma hasa ukiwa ndani ya pango hilo.
Alisema,Hoteli hiyo ina vyumba 16 vya kulala na vyenye hadhi ya madaraja tofauti kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya wageni watakaokwenda na imesaidia sana kutengeneza ajira kwa vijana wa mkoa wa Ruvuma na kufungua fursa na soko la bidhaa mbalimbali kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo kwa kuuza mboga mboga,mayai,kuku na matunda.
Aidha alisema,mpango wa baadaye ni kujenga ukumbi wa kisasa,kuleta huduma jirani ya Supermarket,MinBank na maduka ya vyakula ili kupunguza safari ya kwenda na kurudi mjini ambapo itasaidia sana kuokoa fedha nyingi na muda.
Hata hivyo alisema,Canopies Hoteli inakabiliwa na changamoto chache kati ya hizo ni miundombinu ya barabara,na kuiomba serikali isaidie kujenga barabara ya lami kwani wakati wa masika wageni wanaweza wasiamini kama kuna Hoteli nzuri ya kupumzika.
Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema alisema, Hotel hiyo ni kati ya Hotel zenye hadhi kubwa wilayani Songea ambapo mgeni yoyote anaweza kwenda kwa ajili ya kupumzika.
Alisema,serikali ya wilaya itahakikisha inawaungo mkono wato wote watakaohitaji kwenda Songea kwa ajili ya kuwekeza katika shughuli mbalimbali ikiwamo sekta ya utalii na uwekezaji.
MWISHO.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.