WAZIRI wa Maji Mheshimiwa Jumaa Aweso ametoa zawadi ya mifuko 150 ya saruji kwa Halmashauri tatu za Mkoa wa Ruvuma na fedha kiasi cha shilingi 500,000 kwa wananchi waliotunza vyanzo vya maji.
Waziri Aweso alipofanya ziara ya kikazi mkoani Ruvuma aliahidi kutoa zawadi za saruji mifuko 50 kwa Halmashauri za Nyasa,Halmashauri ya Mbinga mji na Halmashauri ya wilaya ya Mbinga na kutoa fedha shilingi 500,000 kwa Jumuiya moja kati ya sita za watumia maji zilizoundwa mkoani Ruvuma.
Hafla ya kukabidhi zawadi hizo imefanyika kwenye viwanja vya Mkuu wa Wilaya ya Mbinga ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ambaye alikabidhi zawadi hizo kwa niaba ya Waziri wa Maji.
Akitoa taarifa ya Bonde hilo kabla ya kukabidhi zawadi hizo, Mkurugenzi wa Bodi Bonde la Maji la Ziwa Nyasa Mhandisi Arice Engalabeth BONDE la Maji la Ziwa Nyasa lina uwezo wa kutumia maji milimita za ujazo zaidi ya milioni 12 kwa mwaka.
Mhandisi Engalabeth amesema kati ya milimita hizo za maji,meta za ujazo milioni 107 ni za maji chini ya ardhi na kwamba bonde la maji la ziwa Nyasa ni bonde la pili kwa wingi wa maji ya juu ya ardhi kati ya mabonde ya maji tisa yaliyopo nchini.
Hata hivyo amesema bonde la maji la ziwa Nyasa ni la mwisho kwa wingi wa maji chini ya ardhi kati ya mabonde tisa yaliyopo nchini na kwamba bonde hilo lina vituo 54 vya kufuatilia mwenendo wa maji ambapo katika Mkoa wa Ruvuma vituo hivyo vipo katika mito ya Ruhuhu,Ngaka,Lutukira na Lumecha na katika ziwa Nyasa kuna vituo vitatu vinavyofuatilia wingi wa maji kwa usawa wa ziwa.
“Katika Mkoa wa Ruvuma tumeunda Jumuiya sita za watumiaji maji,Mkoa wa Ruvuma una mito mingi ambayo inatiririsha maji,hivyo tunawajibu wa kuhakikisha tunatunza vyanzo vya maji ili viweze kutusaidia kwa maendeleo ya kiuchumi kwa kizazi cha sasa na kijacho’’,alisisitiza Mhandisi Arice.
Amesema Bonde la ziwa Nyasa lina maji mengi ambapo takwimu zilizopo zinaonesha kuwa maji ya bonde la ziwa Nyasa yakigawanywa kila mtu anaweza kupata meta za ujazo 6644 kwa mwaka ukilinganisha na takwimu za kitaifa ambazo zinaonesha mtu mmoja kwa mwaka anapata meta za ujazo 2005.
Akizungumza kabla ya kukabidhi zawadi ya mifuko 150 ya saruji na fedha shilingi 500,000 kwa wananchi waliotunza vyanzo vya maji katika wilaya za Mbinga na Nyasa,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amewaasa wananchi kuendelea kutunza vyanzo vya maji kwa kupanda miti rafiki hasa katika kipindi hiki cha mvua.
Amekemea tabia ya baadhi ya wakazi wa Mbinga kukata miti hadi kwenye vilele vya milima na vyanzo vya maji ambapo amemshukuru Waziri wa Maji Mheshimiwa Jumaa Aweso kwa kutoa zawadi hizo kwa wananchi waliotunza vizuri vyanzo vya maji katika wilaya hizo.
“Zawadi hizo ziwe kichochea kwa wananchi wengine mkoani Ruvuma ili waweze kutunza mazingira na kuhifadhi vyanzo vya maji,tujifunze kutunza na kuhifadhi kile tulichonacho, kila Halmashauri itekeleze lengo la kupanda miti isiyopungua milioni moja kwa mwaka ili tuwe na uhifadhi endelevu’’,alisisitiza RC Thomas.
Ametoa rai kwa wanahabari kuendelea kuandika Makala za kuhamasisha utunzaji wa mazingira, kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji vilivyopo.
Bonde la maji la ziwa Nyasa linapita katika mikoa ya Mbeya, Ruvuma,Songwe na Njombe.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.