CHAMA cha watu wenye walemavu wilayani Mbinga(CHAWATA),kimeiomba serikali kuwapatia wataalam wa lugha za alama waweze kuwasaidia wanapofika katika maeneo ya kutolea huduma na kutoa mchango wao kwenye ujenzi wa Taifa kama ilivyo kwa makundi mengine ya kijamii.
Ombi hilo limetolewa na katibu wa chama hicho Steven Mateso, wakati akitoa taarifa kuhusu mradi wa ustawi,haki na ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu kwa viongozi wa serikali za mitaa,wadau na jamii wilayani humo.
Alisema kukosekana kwa wataalam hao,kumesababisha kukosa baadhi ya haki zao pindi wanapokwenda katika maeneo ya kutolea huduma za kijamii ikiwemo Hospitali,Mahakama,Polisi na ofisi nyingine za umma kwani inakuwa vigumu kueleweka haraka kwa jamii.
Mateso alitaja changamoto nyingine ni kutopewa nafasi pindi wanapojitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi hasa katika maeneo ya vijijini na kukosa elimu ya ujasiriamali na uzalishaji ili kubuni miradi ya kuwaingizia kipato.
Kwa mujibu wa Mateso ni kwamba,hata miundombinu katika majengo ya zamani ya kutolea huduma siyo rafiki kwa walemavu na kutolea mfano ukosefu wa vyoo maalum kwa walemavu.
Alisema,kutoshirikishwa katika vyombo vya maamuzi ngazi ya kijiji,kata na Baraza la madiwani vimekuwa kikwazo kwa kamati za masuala ya watu wenye ulemavu kutekeleza majukumu yake kikamilifu na hivyo kusababisha kundi hilo kubaki nyuma.
Wameiomba serikali kupitia Halmashauri zake,kutenga bajeti ya fedha ili kuiwezesha kamati ya watu wenye ulemavu ziweze kukutana na kujadili masuala muhimu yanayowakabili kama zinavyokutana kamati nyingine.
Aidha alisema,Chawata kimepata ufadhili wa Sh.milioni 33,608,163 kutoka Foundation for Civil Society ili kutekeleza mradi wa ustawi,haki na ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu katika vyombo vya maamuzi katika kata tatu ambazo ni Muungano,Kitura na Mbangamao.
Alitaja kazi zilizofanyika ni kufanya mafunzo kwa wajumbe 90 wa kamati za vijiji kutoka kata tatu za mradi ambapo jumla ya watu wenye ulemavu 33,wenyeviti wa vijiji 11,watendaji 11,watendaji kata 3 madiwani 3 na wenyeviti wa huduma za jamii 11 na wawakilishi walipata mafunzo husika.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbinga Aziza Mangosongo alisema,serikali imeanza imeanza kuboresha miundombinu ili kuwawezesha watu wenye ulemavu kufiki kwenye maeneo ya kutolea huduma kwa urahisi na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa.
Amewahamasisha watu wenye ulemavu kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi,kujiamini na kushiriki katika kazi mbalimbali za kijamii badala ya kujitenga na kujinyanyapaa.
Mangosongo,amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri ya wilaya na Mji Mbinga,kuwaalika watu wenye ulemavu kushiriki vikao mbalimbali vya maamuzi ikiwemo baraza la madiwani na kutenga fedha ili kununua mahitaji na vifaa kama mafuta maalum ya ngozi.
Mangosongo,amewaomba wazazi kutowatenga na kuwafungia ndani watu wenye ulemavu bali kuwapa nafasi na haki zao kama elimu,mavazi na huduma nyingine za kijamii.
Mwakilishi wa Chama cha Walemavu Tanzania Said Kombo Kombo (Manara),amewataka watu wenye ulemavu kutokata tamaa au kubaki nyuma,badala yake kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele na kushiriki kazi mbalimbali za ujenzi wa Taifa.
Amewataka kujiamini na kuaminika wanapopata mikopo kutoka katika taasisi za fedha ikiwemo asilimia kumi inayotolewa na Halmashauri, kwa kurejesha kwa wakati ili kutoa fursa kwa walemavu wengine kukopeshwa badala ya kudhani fedha hizo ni zao.
Amewashauri kuanzisha na kufanya shughuli za kuwaingizia kipato halali kitakachowasaidia kuendesha maisha yao na kuwaondokana na tabia ya kuomba omba kwa watu wengine katika jamii,jambo ambalo ni aibu kubwa kwao.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.