Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma Mhe. Menas Komba amewaonya Wenyeviti wa Vyama vya Msingi vya Ushirika na wadau wa ushirika kujiepusha na udanganifu wa kuiba mazao ya wakulima kwa njia ya kuchezea mizani.
Mhe. Komba ametoa onyo hilo katika kikao cha viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika na wataalamu wa Kilimo na Ushirika wa Halmashauri hiyo kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Halmashauri hiyo uliopo mji mdogo wa Peramiho.
Mhe. Komba amesema kumekuwa na malalmiko mengi toka kwa wakulima wakiwalalamikia viongozi na wadau wa Ushirika kuwaibia mazao yao kwanjia za ujanja ujanja kwakuchezesha mizani kwania mbaya ya kuwadhurumu haki yao.
“Sipendi kusikia malalamiko toka kwa wakulima,kuibiwa mazao kupitia vipimo”,amesema Mhe. komba.
Mhe. Komba amesema Ushirika uliundwa kwa lengo la kusimamia shughuri za wakulima na kuwasaidia hivyo viongozi na wadau wa ushirika wanatakiwa kuwa makini katika kuwahudumia wakulima na kutambua mkulima ndio mtaji mkubwa wa ushirika pasipo mkulima hakuna ushirika.
Mhe. Komba amewaagiza viongozi wa Ushirika wa Halmashauri hiyo kushiriki kikamilifu katika zoezi la kudhibiti utoroshaji wa mazao toka ndani ya Halmashauri kwenda Halmashauri nyingine kwasababu kitendo hicho kinaikosesha Halmashauri mapato yanayotokana na ushuru wa mazao baada ya kutoroshwa.
Ameongeza kwakusema Halmashauri ya Wilaya ya Songea ni Halmashauri yenye rasilimali za kutosha kama vile mito inayotiririsha maji kipindi chote cha mwaka,eneo kubwa linalofaa kwashughuri za kilimo,mvua za kutosha na shehena ya madini ya makaa ya mawe, kinachohitajika ni ushirikiano katika usimamizi na ufuatiliaji kwenye eneo la ukusanyaji wa mapato.
Kwa upande wao viongozi wa vyama hivyo wamesema kutokuwepo kwa bei elekezi ni changamoto kwao kwasababu Makampuni yanakuwa huru kupanga bei wanazozitaka jambo linaoneka kumnyonya mkulima.
Wamesema msimu wa kilimo wa mwaka 2020 /2021 hapakuwa na bei elekezi badala yake Wizara ya Kilimo Ushirika na Umwagiliaji iliagiza mazao yatauzwa kulingana bei ya soko ya siku husika kitendo ambacho kiliwasikitisha wakulima.
Naye Meneja wa Chama kikuu cha Ushirika cha SONAMCU Juma Mwanga ametoa wito kwa wakulima kuzingatia usafi wanapoandaa mazao yao kwa nia ya kuyafikisha sokoni kwa vile makampuni yanayonunua mazao ya wakulima yamekuwa yakifanyabiashara maeneo mengine, mazao yakiwa machafu yanakosa sifa kwamnunuzi.
Mwanga ametoa rai kwa viongozi hao kuonyesha moyo wa uzalendo na kudumisha mshikamano kwakurudisha fadhira kwa wanachama kwenye makazi yao kwakuchangia ujenzi na utekelezaji wa miradi ya kijamii mara wanapolipwa ushuru wao.
Afisa ushirika wa Halmashauri hiyo Damian Lwena amesema ushirika ni nyenzo muhimu sana katika kufanikisha malengo ya wakulima,viongozi wasimamie vema ushirika na kuacha tabia za ubadhirifu wa mali za chama.
Lwena amesema kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2021 /2022 wanakadiria kuvuna tani 3,304 za mazao yanayouzwa kwa mfumo wa stakabadhi gharani ambayo ni ufuta tani 2678, soya tani 473 na mbaazi tani 253.
Halmashauri ya Wilaya ya Songea inajumla ya vyama vya msingi vya ushirika 16 ambavyo vimesajiliwa na vinafanyakazi kwa mujibu wa kanuni,taratibu,na Sheria za nchi.
Imeandikwa na
Jacquelen Clavery
A/habari Songea dc
13/04/2021.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.