BENKI ya NMB imedhamiria kuimarisha sekta ya elimu na afya hapa nchini kutokana na sekta hizo kuwa nguzo ya maendeleo ya jamii kitaifa na kimataifa.
Hayo yamesemwa na Afisa Mkuu Udhibiti na Utekelezaji wa NMB Oscar Nyirenda katika hafla ya kugawa msaada wa bati 240 zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 6.7 zilizotolewa na NMB kwa ajili ya shule ya sekondari ya Litembo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma kwenye maadhimisho ya wiki ya huduma kwa mteja Kanda ya Kusini.
Amesema NMB inaunga mkono Juhudi za serikali ya awamu ya sita katika kusaidia jamii kwa sababu NMB inapata mafanikio makubwa kupitia jamii ya watanzania wote.
‘’Tumekuwa tunaendelea kutoa msaada wa vifaa tiba kama magodoro na vitanda katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma ya afya,pia tumekuwa tunaendelea kusaidia sekta ya elimu ambapo katika Juma hili la huduma kwa wateja NMB imeadhimisha katika Kanda zote ikiwemo ya Kusini’’,alisema .
Amesema Septemba 25 mwaka huu Benki ya NMB ilifanikiwa kukusanya shilingi milioni 400 za kusaidia akinamama wenye tatizo la fistula ambapo walifanikiwa kukusanya michango kwa asilimia 160 ya lengo.
Nyirenda amesema Benki ya NMB kila mwaka imekuwa inatenga asilimia moja ya faida yake ili kuendelea kurudisha sehemu ya faida kwa jamii kwa kusaidia maendeleo ambapo katika kipindi cha miaka kumi iliyopita NMB imepeleka zaidi ya bilioni 12 ili kuchochea kasi ya maendeleo katika jamii.
Hadi sasa NMB ina matawi 225 ambayo yamesambaa katika wilaya zote,pia NMB ina mawakala zaidi ya 6,000 nchini kote na mashine za kutolea fedha zaidi ya 700.
Imeandikwa na Albano Midelo,Mbinga
Oktoba 6,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.