Waziri wa Maji Mheshimiwa Juma Aweso,akiondoa kitambaa kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa mradi wa maji Ndelenyuma-Lutukila unaotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini(RUWASA) kwa gharama ya Sh.bilioni 1.6,kushoto Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mwajuma Waziri na kulia Mbunge wa Jimbo la Madaba Dkt Joseph Mhagama.
WIZARA ya Maji itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika vijiji mbalimbali nchini, ili kuwaondolea wananchi adha ya kuamka usiku wa manane na kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya familia zao.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Maji Mheshimiwa Juma Aweso,baada ya kuweka jiwe la msingi ujenzi wa mradi wa maji wa Lutikira-Ndelenyuma kata ya Mkongotema Halmashauri ya Madaba mkoani Ruvuma unaotekelezwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)kwa gharama ya Sh.1,614,363,301.70.
“Sitokuwa kikwazo kwa wananchi wa Jimbo la Madaba kuhusu huduma ya maji safi na salama,wizara ya maji tumejipanga kuhakikisha tunafikisha huduma ya maji safi na salama kwenye maeneo yote yenye changamoto ya maji ili kutoa fursa kwa wananchi kufanya shughuli zao za maendeleo”alisema.
Waziri Aweso,amemtaka Mkandaras na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Songea Mhandisi Mathias Charles,kuhakikisha mradi huo unakamilika haraka ili wananchi waweze kupata huduma ya maji safi na salama badala ya kuendelea kutumia maji kutoka kwenye vyanzo vya asili.
Alisema,mradi wa maji Ndelenyuma Lutukira utasaidia wananchi hasa akina mama ambao ni wahanga wakubwa kwa kuamka usiku na kuwaacha waume zao pindi wanapokwenda kutafuta maji kwa matumizi ya familia zao.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mwajuma Waziri,amewataka wananchi wa vijiji hivyo kutunza mradi huo na vyanzo vya maji ili uwe endelevu kwa manufaa yao na kizazi kijacho mradi.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Songea Mhandisi Mathias Charles alisema,Mradi huo umefikia asilimia 86.7 ya utekelezaji wake ulitarajia kukamilika mwezi Disemba 2022, lakini kutokana na changamoto mbalimbali ulishindwa kukamilika kwa muda uliopangwa hali iliyosababisha Mkandarasi kuomba kuongezewa muda tarehe 16 Oktoba mwaka huu.
Alisema,chanzo cha maji kinachotumika ni chemchem yenye uwezo wa kuzalisha lita 1,123,200 kwa siku wakati mahitaji ya maji kwa wakazi wa vijiji hivyo ni lita 298,000.
Mathias alitaja kazi zilizopangwa kutekelezwa katika mradi huo ni ujenzi wa nyumba ya mtambo wa kusukuma maji,ujenzi wa tenki la maji la ujazo wa lita 150,000 katika mnara wa mita 6,kujenga uzio na vituo 15 vya kuchotea maji.
Aidha alitaja kazi nyingine zilizopangwa kutekelezwa ni kuchimba mtaro,kulaza na kuunganisha bomba umbali wa kilometa 23.768,ununuzi na ufungaji wa pampu,kuunganisha umeme kwenda kwenye nyumba ya mtambo,ujenzi wa chanzo na tenki la chini la ujazo wa lita 50,000.
Alieleza kuwa,hadi sasa Sh.milioni 768,110,151.38 kati ya Sh.bilioni 1.6 zimetumika na kazi zinazoendelea kwa sasa ni kufanya majaribio ya kusambaza maji kwenye maeneo yote yaliyopangwa.
Hata hivyo alieleza kuwa,katika utekelezaji wa mradi kiasi cha Sh.414,638,635.00 zimeongezeka kutokana na kuongezeka kwa kazi ambazo zilitakiwa zifanyike kwenye maeneo ambayo hayakuwafikiwa na miradi na ujenzi wa tenki ambalo halikuwepo kwenye mkataba.
Mbunge wa Jimbo la Madaba Dkt Joseph Mhagama,ameishukuru serikali kwa kutoa fedha nyingi ambazo zimetumika kutekeleza miradi ya maji katika vijiji mbalimbali vya Jimbo hilo ikiwemo mradi wa maji Mtyangimbole unaotekelezwa kwa gharama ya Sh.bilioni 5.
Mhagama alitaja miradi mingine inayotekelezwa ni pamoja na mradi wa maji Mbangamawe wenye thamani ya Sh.milioni 545 na mradi wa Ngadinda unaotekelezwa kwa Sh.bilioni 1.4.
Awali Diwani wa kata ya Mkongotema Vestus Mfikwa alisema,mradi huo umeanza kuleta Amani na furaha kwa wananchi,kwani tangu cha Ndelenyuma kilipoanzishwa miaka mitano iliyopita hakijawahi kupata maji ya bomba badala yake wananchi walitumia maji ya mito na visima.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.